Languages فارسی العربية English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsch español فارسى درى РУС
Scroll down
HISTORIA YA WATUKUFU

mubahala

2016/11/12

mubahala

MUBAHALA

Wawakilishi Wa Najraan Mjini Madina

Nchi yenye kupendeza ya Najraan iliyokuwa na vijiji sabini na viwili iko kwenye mpaka wa Hijaz na Yemen.

Katika siku za awali za Uislamu hili lilikuwa eneo pekee nchini Hijaz lililokuwa likikaliwa na Wakristo, ambao kwa sababu fulani fulani waliacha ibada ya masanamu na kuingia dini ya Ukristo.1

Sambamba na barua ambazo Mtume wa Uislamu aliwaandikia wakuu wa nchi mbalimbali za ulimwenguni, vilevile alimwandikia barua Abu Harith, Askofu wa Najraan, na kwa barua ile aliwalingania kwenye Uislamu watu wa eneo lile. Maneno ya barua ile yalikuwa hivi: “Kwa jina la Mola wa Ibrahim, Ishaaq, na Ya’aqub.

Hii ni barua itokayo kwa Muhammad Mtume na Mjumbe wa Allah iendayo kwa Askofu wa Najraan. Ninamsifu na kumtukuza Mola wa Ibrahim, Ishaaq na Ya’qub, na ninakuiteni nyote kumwabudu Allah badala ya kuviabudu viumbe Vyake, ili muweze kutoka chini ya ulinzi wa viumbe wa Allah na kuchukua nafasi chini ya ulinzi wa Allah Mwenyewe.

Na kama hamtaukubali mwito wangu, basi ni lazima (angalau) kulipa Jizyah(kodi) kwenye serikali ya Kiislamu (kwa malipo ambayo itachukua jukumu la kuhifadhi uhai na mali zenu), na mkishindwa kufanya hivyo, mnaonywa juu ya matokeo ya hatari.”2

Baadhi ya vitabu vya Kishia vinaongeza kusema kwamba, vilevile Mtume (s.a.w.w.) aliandika kwenye barua hii, aya ya Qur’ani ihusianayo na watu wa Kitabu ambayo ndani yake wote wameitwa kumwabudu Allah Aliye Mmoja tu. Hapa aya ya sitini na nne ya Sura Aali Imran ilizungumziwa: “Sema: Enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu naninyi: Ya kwamba tusimwabudu yeyote ila Allah, wala tusimshirikishe na chochote, wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa miungu badala ya Allah….”

Mjumbe wa Mtume (s.a.w.w.) aliwasili Najraan na kumpa yule Askofu ile barua. Aliisoma barua ile kwa uangalifu mkubwa, na kisha ili kuweza kutoa uamuzi, aliitisha mkutano wa viongozi wa kidini na wa kilimwengu ili awatake ushauri. Mmoja wa wale watu walioitwa kutoa ushauri alikuwa ni mtu mmoja aliyeitwa Shurahbil aliyekuwa maarufu kwa elimu wake, hekima na ujuzi.

Alipokuwa akimjibu yule Askofu, alisema hivi: “Ujuzi wangu wa mambo ya kidini ni haba mno, na hivyo basi mimi sina haki ya kuzitoa fikiza zangu juu ya mambo hayo, lakini kama ukinitaka ushauri juu ya mambo mengine yasiyokuwa haya ninaweza kutoa maoni yangu juu ya utatuzi wa tatizo hilo. Hata hivyo, ninalazimika kusema jambo moja ambalo ni kwamba kila mara tumekuwa tukisikia kutoka kwa viongozi wetu kwamba kazi ya Utume itahamishwa kutoka kwenye kizazi cha Ishaaq kwenda kwenye kizazi cha Ismaili na kwamba si jambo lisilowezekana kwamba Muhammad ambaye yu kizazi cha Ismail, kuwa ndiye yule Nabii aliyeahidiwa!”

Ile halmashauri ya ushauri iliamua kwamba kikundi cha watu kiende Madina wakiwa ni wawakilishi wa Najraan ili waweze kuonana na Muhammad na kuzichunguza habari za Utume wake. Waliteuliwa watu sita waliokuwa wataalamu na wenye hekima zaidi kutoka miongoni mwa watu wa Najraan. Kikundi hiki kiliongozwa na viongozi wa kidini watatu ambao majina yao yalikuwa haya:

Abu Harith bin Alqamah, Askofu Mkuu wa Najraan aliyekuwa mwakilishi maalumu wa Kanisa Katoliki nchini Hijaz.

Abdul Masih, Mkuu wa kamati ya wawakilishi, aliyekuwa maarufu kwa hekima zake, busara na uzoefu.

Ayham, mtu mzima aliyekuwa akichukuliwa kuwa yu mtu mwenye kuheshimiwa wa jumuiya ya watu wa Najraan.3

Wajumbe hawa waliwasili msikitini wakati wa alasiri wakiwa wamevaa nguo za hariri, pete za dhahabu na misalaba shingoni mwao, wakamsalimu Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, hali yao yenye kuchukiza na isiyo sahihi, na pia ikiwa ni msikitini, ilimchukiza Mtume (s.a.w.w.). Walitambua kwamba wamemuudhi, lakini hawakuelewa ni kipi kilichomuudhi.

Hivyo basi, upesi sana walionana na Uthman bin Affan na Abdur-Rahman bin Awf, waliokuwa wakiwajua kabla ya hapo na wakawaeleza jambo lile. Uthman na Abdur-Rahman waliwashauri kwamba ufumbuzi wa tatizo lao uko mikononi mwa Sayyidna Ali bin Abu Twalib (as). Hapo wakakutana na Amirul-Mu’minin (a.s.), naye akiwajibu, akiwaambia: “Lazima mbadilishe mavazi yenu na kwenda kwa Mtume mkiwa mmevaa nguo zilizo rahisi na bila ya kuwa na mapambo yoyote yale. Hapo mtapata heshima na taadhima.”

Wale wawakilishi wa Najraan wakavaa nguo rahisi na wakavua zile pete na kisha wakamjia Mtume (s.a.w.w.). Mtume (s.a.w.w.) akaijibu salam yao kwa heshima kuu na vilevile alizipokea baadhi ya zawadi walizozileta. Kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya pande zote mbili wale wajumbe walisema kwamba muda wao wa sala ulikuwa umewadia, Mtume (s.a.w.w.) aliwaruhusu kusali sala zao msikitini mle wakizielekeza nyuso zao upande wa Mashariki.4

Wajumbe Wa Kutoka Najraan Wajadiliana Na Mtume (S.A.W.W.)

Idadi kubwa ya waandishi wa wasifu, wanahadithi na wanahistoria wa Kiislamu, wameyanukuu maneno ya mazungumzo baina ya wawakilishi wa Najraan na Mtume (s.a.w.w.). Hata hivyo, Marehemu Sayyid bin Taawus ameyanukuu maneno ya majadiliano yale na tukio la Mubahila (Maapizano) katika hali iliyo sahihi zaidi, kwa upana zaidi na kwa namna ya maelezo marefu zaidi, ukilinganisha na waandishi wengine. Ameyanukuu mambo yote na Mubahila tangu mwanzoni hadi mwishoni kutika kitabu kiitwacho “Kitabu Mubaahila’ cha Muhammad bin Abdul Muttalib Shabaan na ‘Kitab ‘Amaali Dhil Haj cha Hasan bin Ismail.5

Hata hivyo, ni nje ya upeo wa kitabu hiki kutoa maelezo marefu ya tukio hili la kihistoria, ambalo kwa bahati mbaya hata halikudokezwa na baadhi ya waandishi wa wasifu. Kwa hiyo, tunataja hapa mambo machache juu ya mazungumzo yale, kama yalivyoelezwa na Halabi katika kitabu chake kiitwachoSiiratu.6

Mtume (s.a.w.w.): “Ninakuiteni kwenye dini ya Upweke wa Allah na ibada ya Allah Aliye Mmoja tu na kuzitii amri Zake.” Kisha Mtume (s.a.w.w.) akazisoma baadhi ya aya za Qur’ani mbele yao.

Wajumbe wa Najraan: “Kama Uislamu una maana ya kumwamini Mola wa Ulimwengu, sisi tayari tumeshamwamini na tunazitekeleza amri zake.”

Mtume (s.a.w.w.): “Uislamu una dalili chache na baadhi ya matendo yenu yanaonyesha kwamba hamuuamini Uislamu. Mnawezaje kusema kwamba mnamwanini Allah Aliye Mmoja tu na hali mnauabudu msalaba na hamjiepushi na nyama ya nguruwe na mnaamini kwamba Allah anaye mwana?”

Wajumbe wa Najraan: “Tunamwamini yeye (yaani Isa) kuwa yu mungu kwa sababu aliwafufua wafu, aliwaponya wagonjwa, alimtengeneza ndege kutokana na udongo na kumfanya aruke, na mambo yote haya yaonyesha kwamba yeye ni mungu.”

Mtume (s.a.w.w.): “Hapana! Yeye yu mja wa Allah naye yu kiumbe chake. Allah Alimweka kwenye tumbo la uzazi la Maryamu. Na uwezo na nguvu yote hii alipewa na Allah.”

Mjumbe mmoja: “Ndio! Yeye yu mwana wa Muumba, kwa sababu Maryamu alimzaa bila ya mume yeyote, na hivyo basi, ni muhimu kwamba baba yake ni Yeye yule Mola wa ulimwengu.”

Kufikia hapa, Malaika Mkuu Jibriil (a.s.) alishuka na kumshauri Mtume (s.a.w.w.) awaambie: “Kwa mujibu wa maoni hayo, hali ya Isa ni kama ile ya Adamu aliyeumbwa na Allah kwa nguvu Zake zisizo kifani, kutokana na udongo bila ya yeye kuwa na baba wala mama.7 Kama mtu kutokuwa na baba ni uthibitisho wa kuwa kwake mwana wa Mungu, basi Adamu anastahiki zaidi cheo hiki kwa sababu yeye hana baba wala mama.”

Wajumbe wa Najraan: “Maneno yako hayatutoshelezi. Njia iliyo bora zaidi ya kulitatua swali hili ni ile ya kwamba tufanye Mubahala (Maapizano) baina yetu katika muda utakaowekwa na kumlaani yule aliye mwongo baina yetu na tumwombe Allah kwamba Amwangamize yule aliye mwongo.”8

Wakati huo huo Malaika Mkuu Jibriil (a.s.) alikuja na akaileta ile Aya ihusianayo na Mubaahila na kuiwasilisha kwa Mtume (s.a.w.w.) amri ya Allah kwamba yeye Mtume (s.a.w.w.) afanye hicho kiapo na wale washindanao na kumbishia, na makundi yote mawili yaombe kwa Allah kwamba Amnyime yule mwongo baraka Yake. Qur’ani Tukufu inasema: “Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zetu na wanawake zenu, na nafsi zetu na nyinyi nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Allah iwashukie waongo.” (Sura AaliImran 3:61).

Pande zote mbili zilikubali kulitatua suala hili kwa njia ya kulaaniana, na iliamuliwa kwamba wote wajiweke tayari kwa ajili ya maapizano hayo katika siku inayofuata.

mubahala sehemu ya pili